Our school

Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela, Arusha, Daktari Dina Machuve, amefanikiwa kupata ufadhili wa Dola 50,000 fedha za kimarekani kwa ajili ya kukamilisha mfumo unaotumia tekinolojia ya akilibandia (Artificial Intelligency) kutambua dalili za awali za magonjwa yanayo athiri kuku mara kwa mara. Magonjwa hayo ni pamoja na kideri na homa ya matumbo(typhoid).

Fedha hizo alizipata Dkt Machuve baada ya kuibuka mmojawapo wa washindi 20 walioshindanishwa kutoka nchi 14 zinazoendelea ikiwemo, Tanzania, Ghana, Sir-Lanka, Bangladesh, Guatemala, Benin, Bolivia, Kenya, Uganda, Burkina Faso, Nepal, Madagascar, Ethiopia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya watu wa Laos. Mashindano hayo huendeshwa na shirika la kuinua vipaji vya wanasayansi wanawake katika nchi zinazoendelea yaani “Organisation for Women in Science for developing World (OWSD). Shirika hilo hupitia na kujiridhisha viwango vya ubunifu kiteknolojia na kisayansi pamoja na uwezo wa wanawake wa kutumia teknolojia katika kutatua changamoto zinazoikabili jamii ya nchi zinazoendelea. Fedha hizi za tafiti zitamwezesha Daktari Dina Machuve kufikia malengo ya kukamilisha utengenezaji wa mfumo huo hadi kuufikisha kwa wafugaji, maafisa ugani pamoja na wadau wa sekta ya ufugaji kuku nchini.

”Nilipoanza utafiti huu, ilinibidi nivae viatu vya wafugaji, kwa hiyo nilianza kufuga kuku mwenyewe lengo likiwa kuhakikisha kuwa ninajifunza na kuelewa changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo wafugaji na kuutumia mfumo huo kuona kama utatatua changamoto husika katika mradi wangu kuanza. Hatua hiii ilibadilisha mtazamo wangujuu ya ufugaji na kuniwezesha kujua undani wa tatizo na teknolojia inyoweza kutatua changamoto za wafugaji pamoja na namna sahihi ya kufanya kazi na wafugaji” alieleza Daktari Dina Machuve.

Mkulima anapokuwa na mfumo huo kwenye simu yake (Mobile App), atatakiwa kupiga picha ya kinyesi cha kuku, baada ya hapo mfumo huo utatoa taarifa kama kuku huyoana ugonjwa kati ya magonjwa matatu au la. Hii ni njia ya kisasa rahisi na ya muda mfupi sana ambayo itarahisisha ugunduzi wa ugonjwa mapema sana akabla kuku hawajaathirika kuliko mifumo inayotumika kwa sasa ambayo inahusisha kuchukuliwa na kupeleka sampuli maabara kwa ajili ya vipimo shughuli ambayo hutumia takribani wiki moja. Sambamba na zoezi hilo kuchukuwa muda mrefu, pia linakuwa ghali kwa kuwa huhusisha kumlipa daktari wa mifungo pamoja na kulipia vipimo.

”Hakika ninaona kwamba mfumo huu utakapo malizika utawasaidia jamii ya wafugaji pamoja na maafisa ugani katika kuepukana na hasara wanayopata kutokana na magonjwa hayo, wataweza kufanya ufugaji wenye tija hivyo kujiongezea kipato na kipato cha taifa hasa wakati huu ambapo tunaelekea uchumi wa kati wenye kutegemea viwanda” aliongeza Daktari Dina Machuve.

Ufadhili huo wa dola 50,000 fedha za kimarekani utatumika kumalizia matengenezo ya mfumo pamoja na kuwanufaisha wafugaji katika mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro kama hatua ya kwanza ya mradi. Mfumo unaweza kutumika Tanzania, Afrika Mashariki na hata nje ya mipaka ya Afrika Mashariki kwa kuwa maeneo mengi yana changamoto ya magonjwa yaliyokuwa yakikusudiwa kutambuliwa.

Back to top